Waziri wa usalama wa Israel Yuval Steinitz amesema leo kuwa mswada wa azimio uliowasilishwa kwa niaba ya Palestina katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni tangazo la vita. Waziri Steinitz amesema hiyo si hatua ya amani , bali ni hatua ya vita ambayo Palestina inaelekeza.
Waziri Steinitz ameiambia radio ya Israel, iwapo mamlaka ya Palestina itaendelea kukandamiza majadiliano ya amani na kuelekea katika hatua za kipekee za kidiplomasia dhidi ya Israel , nchi hiyo itafikiria fursa zote, ikiwa ni pamoja na kuivunja mamlaka hiyo.
Jordan , kwa niaba ya wapalestina, imewasilisha mswada wa mwisho jana, ambao unatoa wito wa makubaliano ya amani katika muda wa mwaka mmoja baada ya mswada huo kuidhinishwa na Israel iondoe majeshi yake kutoka katika ardhi inayoikalia kabla ya mwisho wa mwaka 2017.
Israel inaogopa kufikishwa mswada huo, kwani hatua hiyo itapelekea Israel kuwa dhaifu, hivyo Israel na swahiba wake Marekani wanajaribu kila njia kuishawizi Palestina kwa ahadi za kitoto ili iachane na mpango huo, na kuiacha Israel iendelee kukalia ardhi za Palestina ilizozinyang’anya kwa nguvu.